Thursday, May 30, 2013

YANGA YAIKABIDHI MIL 25 NA TBL

Meneja wa Bia ya Kilimanjaro George Kavishe kushoto akimkabidhi mfano wa hundi Katibu Mkuu wa Young Africans Lawrence Mwalusako leo katika hafla iliyofanyika katika kiwanda cha bia TBL IIlala.
Kilimanjaro Premium Lager – wadhamini wakuu wa timu ya Yanga  imetoa kiasi cha shilingi milioni 25 kama zawadi kwa timu hiyo kwa kushinda Ligi Kuu ya Vodacom 2012/2013. 
 
Akikabidhi hundi ya Sh milioni 25 kwa Yanga SC, Meneja wa bia ya Kilimanjaro Premium Lager, George Kavishe alisema Kilimanjaro Premium Lager imefurahishwa sana na ushindi wa timu ya Yanga na kusema imejizatiti kikamilifu kuisaidia timu ambayo imeibuka bingwa katika ligi yenye ushindani mkubwa kutokana na kuibuka kwa timu mpya zenye nguvu.
    
“Yanga imekuwa ikicheza mpira mzuri kipindi chote cha msimu wa ligi kuu, na sio ajabu wao kuibuka washindi wa Ligi hii. Napenda kuwapongeza wachezaji wa Yanga, kocha na Uongozi mzima wa Yanga kwa  matokeo mazuri ya kushinda Ligi kuu kwa mara ya 24 sasa.”
 
Kavishe aliongeza kuwa zawadi hiyo ni sehemu ya sh bilioni 1.5 ya udhamini wa Kilimanjaro Premium Lager kwa Yanga   na imetolewa kwa lengo la kuhamasisha klabu kujitahidi kwa ushindi zaidi na kusaidia klabu katika maandalizi yake kwa ajili ya mashindano ya kimataifa ambayo tayari Yanga ina sifa za kushiriki kutokana na ubingwa waliojipatia.
 
Akipokea hundi hiyo, Katibu mkuu wa Yanga , Bwana Lawrence Mwalusako alisema Yanga inaishukuru sana Kilimanjaro Premium Lager kwa mchango wao. Aliongeza kuwa Yanga ni timu nzuri na yenye nguvu kutokana na uongozi imara pamoja na udhamini mkubwa kwa bia ya Kilimanjaro Premium Lager.  
 
‘‘Mafanikio yetu ya uwanjani ni kielelezo cha mafanikio ya kampuni na pia (TBL) na bia ya Kilimanjaro Premium Lager kwa ujumla ambayo imekuwa ikitusaidia sana. Kilimanjaro  Premium Lager imetoa mchango mkubwa sana katika kuipa timu msukumo uliopelekea mafanikio haya,’’ alisema Mwalusako.
 
Mwalusako aliongeza “Yanga sasa ina nafasi ya kuonekana kwenye jukwaa la kimataifa la soka kutokana na mafanikio haya’’.  “Tunaamini kuwa kutokana na udhamini wa Kilimanjaro Premium Lager tutaendelea kukua na kufanikiwa.’’
 
Yanga itawakilisha Tanzania katika michuano ya Klabu Bingwa Afrika na Kombe la Kagame.
MWISHO.

No comments:

Post a Comment

LinkWithin

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...