Monday, May 6, 2013

MBATIA AZIDI KUIBANA SERIKALI,AMSHANGAA KAWAMBWA KUTOJIUZULU.

SIKU moja baada ya serikali kufuta matokeo ya mtihani wa kidato cha nne na kuamuru yaandaliwe upya, Mwenyekiti wa Chama cha NCCR-Mageuzi, James Mbatia, ameshangaa kuona Waziri Kawambwa hajiuzulu na ametaka wazazi wa wanafunzi waliojinyonga kwa matokeo hayo walipwe fidia.
Wakati akitaka wanafunzi hao walipwe fidia, pia Mbatia alimshangaa Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dk. Shukuru Kawambwa, akihoji anasubiri nini kung’atuka wakati kuna wanafunzi wamepoteza maisha kwa uzembe wao.
Alisema Kawambwa anapaswa kujiuzulu kwani Katibu Mkuu wa Baraza la Mitihani nchini, Joyce Ndalichako, hawezi kufanya mabadiliko makubwa ya aina hiyo bila kuishirikisha wizara.
Akizungumza na waandishi wa habari jana mjini hapa, Mbatia ambaye pia ni Mbunge wa kuteuliwa alisema serikali imekuja na majibu rahisi kwenye jambo gumu, kwani uamuzi wa kufuta na kuandaa upya matokeo hayo kwa utaratibu wa mwaka 2011, hauleti ufumbuzi wa mfumo wa elimu.
“Tume imekuja na majibu mepesi sana kwenye tatizo kubwa. Wanafunzi wamejiua kwa msongo wa mawazo, wengine wamekata tamaa na kuamua kuolewa, wengine kupata ujauzito, leo kwa uzembe wao wanataka kuwafaulisha wanafunzi ili kupata sifa kisiasa, haiwezekani,” alisema.
Akichambua maoni ya tume hiyo, alisema imeibua hoja ambazo yeye aliziwasilisha bungeni kupitia hoja yake binafsi ambayo ilizimwa na wabunge wa CCM kwa sababu za kulinda masilahi ya chama chao.
Alilishambulia Bunge kuwa limekuwa chanzo cha matatizo mengi kutokana na ubinafsi wa vyama bila kujali masilahi ya taifa.
“Bunge linaangamiza taifa kwa sababu ya itikadi. Hizi itikadi za vyama zinaliangamiza taifa. Kuna umimi, ubinafsi kwenye mambo ya masilahi ya taifa. Nawataka wabunge watoke usingizini,” alisema Mbatia.
Juzi serikali ilitangaza kufuta matokeo ya kidato cha nne ya mwaka 2012 na kuagiza yaandaliwe upya.
Uamuzi huo mgumu ulitangazwa bungeni na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge), William Lukuvi.
Akisoma tamko hilo kwa niaba ya Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, Lukuvi alisema uamuzi huo wa serikali umetokana na mapendekezo ya tume ya waziri mkuu iliyoundwa kuchunguza chanzo cha matokeo ya kidato cha nne mwaka jana kuporomoka kwa kiwango cha kutisha.
Matokeo ya mitihani ya kidato cha nne mwaka 2012 yalionesha kuwa kiwango cha ufaulu kimeshuka kwa kiwango kikubwa ikilinganishwa na miaka ya hivi karibuni.
Matokeo yaliyotangazwa hivi karibuni, yalionesha kwamba kati ya wanafunzi 367,756 waliofanya mtihani huo, watahiniwa 126,847 ndio waliofaulu.
Katika idadi hii, wanafunzi waliofaulu katika daraja la kwanza hadi la tatu ni 23,520, sawa na asilimia 6.4 na daraja la nne ni 103,327, sawa na asilimia 28.1.
Watahiniwa 240,909, sawa na asilimia 65.5 ya wanafunzi wote, waliofanya mtihani wa kidato cha nne mwaka 2012, walipata daraja sifuri.

Kuendela,bofya Read More
BAVICHA nao wanena
Lucy Ngowi anaripoti kuwa, Baraza la Vijana wa CHADEMA (BAVICHA), limemtaka Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dk. Shukuru Kawambwa na wasaidizi wake kujiuzulu mara moja ili kupisha wenye uwezo wa kusimamia sekta hiyo.
Katibu Mkuu wa BAVICHA, Deogratias Munishi, alisema hayo katika tamko alilolitoa jana baada ya Tume ya Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, kutoa ripoti ya awali kuhusu sakata la kufeli vibaya kwa wanafunzi waliofanya mtihani wa kidato cha nne mwaka jana.
Akinukuu moja ya sababu za kushindwa kwa wanafunzi hao, Munishi alisema ni kutumika kwa alama mpya tofauti na miaka ya nyuma bila taarifa kwa walengwa.
Alisema kuwa huo ni muendelezo wa siasa na mzaha kwa Watanzania kunakofanywa na serikali ya CCM kwenye masuala nyeti.
“BAVICHA inasisitiza Waziri Kawambwa na wasaidizi wake wajiuzulu nyadhifa zao ili kupisha watu wenye uwezo wa kusimamia sekta hii na taasisi zilizo chini yake,” alisema Munishi.
Aliongeza kuwa viwango hivyo vipya vilivyowekwa na Baraza la Mitihani bila kushirikisha wadau ni kiashiria cha uzembe uliokithiri.
“Kama Baraza lilifanya maamuzi hayo bila waziri kujua nako kunaashiria uzembe uliobobea wa waziri huyu wa kushindwa kujua kinachofanyika na taasisi zilizo chini yake na kwa maana hiyo ni mzigo kwa taifa,” alisema.
Kwa mujibu wa Munishi, suala hilo limeleta athari kwa wanafunzi, kwani baadhi yao wamepoteza maisha kwa kujinyonga.
 
SOURCE: chadema SOCIAL MEDIA.

No comments:

Post a Comment

LinkWithin

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...